HOSPITALI YA MOUNT MERU YAWAZAWADIA WATUMISHI HODARI

Posted on: August 22nd, 2021

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru), Dkt. Alex Ernest leo Agosti 24, 2021 amewatunuku vyeti vya shukrani na pesa taslimu Watumishi 76 kutokana na juhudi na ufanisi waliouonesha katika kuhudumia wagonjwa hospitalini hapo.

Dkt. Ernest ametoa motisha hiyo leo Agosti 24, 2021 katika hospitali hiyo Jijini Arusha ambapo kati ya watumishi hao, 69 ni Wahudumu wa Afya waliokuwa mstari wa mbele kwenye kuhudumia wagonjwa wa UVIKO-19, saba ni watumishi bora wa hospitali kutoka Idara mbalimbali zilizopo hospitalini na kwa Idara bora kwa utendaji wa kazi ambapo Idara ya magonjwa ya dharura imeibuka kinara kwa mwezi wa Julai mwaka 2021.

Mbali na kuwatunuku vyeti na pesa taslimu, Mganga Mfawidhi pia amewapongeza  wahudumu hao na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali katika hospitali hiyo na kusisitiza watumishi wengine kuiga mfano huo ili kuboresha huduma katika hospitali hiyo.

“Napenda kuwapongeza watumishi wote wa hospitali kwa kujitoa kwa moyo mmoja kuhudumia wagonjwa wanaofika kwenye hospitali yetu lakini pia natoa shukrani za dhati kwa wahudumu wa afya waliochaguliwa kama watumishi bora wa hospitali na ninaahidi jitihada zenu hatutazifumbia macho”, alisisitiza Dkt. Ernest.

Zoezi la kuwazawadia watumishi wa hospitali ya Mount Meru ni endelevu na litakuwa likifanyika kila mwezi ikiwa ni sehemu ya kutoa motisha kwa watumishi ili kuongeza juhudi na ufanisi katika kutoa huduma hospitalini hapo pamoja na kutambua mchango wao kwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha.