UWEKAJI JIWE LA MSINGI UJENZI WA JENGO LA MIFUPA

Posted on: June 16th, 2021

Serikali ipo tayari kushirikiana na taasisi ya  Kili Clinicians Association kutoka Chuo Kikuu cha Barcelona Spain katika kuhakikisha Hospitali ya Mt.Meru inakuwa chuo cha kufundishia.

Yamesemwa hayo na Kaimu Mkurugenzi idara ya tiba kutoka Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Vivian Wonanji katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la uboreshaji wa jengo ya Mifupa Hospitali ya Mt.Meru.

Amesema maendeleo yoyote yanaletwa na ushirikiano ili kuweza kusonga mbele zaidi.

Wizara utatoa ushirikiano mkubwa kwa taasisi hiyo ya Kili clinicians Associations na uwongozi mzima wa Hospitali ya Mt. Meru katika kuboresha zaidi na kupanua huduma zake.

Prof. Jaime Miranda kutoka taasisi ya Kili Clinicians Associations amesema  taasisi yake iliona umuhimu wa kuisaidia Hospitali ya Mt. Meru kupanua huduma zake ili ziwe bora na kuweza kuwafikia watu wengi.

Amesema kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo watanzania watahakikisha ndoto yao inakamilika kwa kuifanya Hospitali ya Mt. Meru kuwa Chuo cha kufundishia cha mfano.

Nae, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mt. Meru Dkt. Alex Ernest amesema mradi huo utagharimu zaidi ya Milioni 185 na utakamilika kati ya miezi 6 hadi 12.

Amesema kukamilika kwa jengo hilo kutapunguza sana foleni kubwa ya wagonjwa iliyokuwepo katika huduma ya upasuaji.

Pia, itapunguza ucheleweshwaji wa upatikanaji wa huduma na itaboresha huduma za Mifupa kwa ujumla kwani vifaa vya kisasa vitatumika.

Dkt. Ernest amesema mbali na kushirikiana na taasisi hiyo katika kuboresha jengo la Mifupa pia watashirikiana katika sekta ya utafiti  na ufundishaji hasa kwenye huduma za Meno kwa kuifanya Hospitali hiyo kuwa Chuo Cha kufundisha madaktari wa Meno.

Maboresho ya jengo la Mifupa ni juhudi zilizofanywa na Mkuu wa kitengo hicho Dkt. Alex Mashala katika kuhakikisha kitengo hicho kinatoa huduma iliyobora na ya kisasa kwa wananchi wote.